Thursday, August 11, 2011

Balaa la Mafuta Mchango wa Mh Zitto Bungeni

MHE. KABWE Z. ZITTO: 
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida tumezoea kuona wafanyakazi wakigoma kudai maslahi yao pale ambapo wanapoona maslahi yao hayatekelezwi na waajiri.  Wanaita industrial action.  Hatujawahi kuona kwa muda mrefu wafanya biashara wakifanya industrial action na tulipoamua ku-liberalize kufungua uchumi wetu kuwa uchumi wa soko tulitoa haki kwa wafanya biashara kufanya kazi kwa mujibu wa soko.  Lakini kamwe hatukuondoa uwajibikaji wa Serikali. 

Bado responsibility ya Serikali kulinda raia wake ilibakia  ni jukumu la Serikali.  Wafanya biashara kwa kutumia cartel yao wameamua kukiuka maagizo ya chombo cha Serikali.  Hatupaswi kuwa na maneno matamu ya aina yoyote dhidi yao.  Ni lazima ionekane kuna Serikali.  Ni lazima ionekane kuna dola.  Ni lazima ionekane kuna uwajibikaji ambao vyombo vya Serikali inafanya kulinda raia.  Sheria ya EWURA imetoa nafasi, imetoa hadhi ya EWURA kulinda walaji na imesisitiza kulinda walaji wa hali ya chini.  Kifungu cha 6(B) cha Sheria ya UWURA.
Leo wananchi wetu Dar es Salaam na miji mingine ya nchi wanahangaika.  Hawawezi kwenda makazini kwenda kufanya kazi za kuzalisha mali.  Wakienda kwenye madala dala hivi sasa nasikia daladala zimepandisha bei.   Kule Kigoma leo ni siku ya nne hakuna umeme.  Kwa sababu hakuna mafuta. Wafanya biashara wa mafuta wanai-hold nchi, hatuwezi kukubali.  Kama nilivyosema in a democracy wafanya biashara wana haki zao kama wafanya biashara.  Lakini Serikali ina majukumu yake na wajibu wake kama Serikali.
Naiomba na ninapenda nilishawishi Bunge, kwamba EWURA leo wa-order wafanya biashara wote wa mafuta wa-release mafuta.  Atakayepinga anyang’anywe leseni mara moja.  Natoa ujumbe kwa wananchi wetu inawezekana maamuzi haya yakawa yakawaletea shida.  Haitakuwa mara ya kwanza wananchi wetu wanapata shida.  Tulikwenda vitani kupiga na Nduli Iddi Amini hatukuwa na uwezo, hatukuwa na vifaa kama alivyokuwa navyo yeye.  Hatukuwa na wakubwa wanaotuunga mkono kama alivyokuwa anaungwa mkono yeye.  Wafanya biashara binafsi walitoa magari yao. Wanajeshi na mgambo walikuwa mobilized tukaenda vitani tukampiga Nduli tukamtoa na tukamtoa Uganda.  
Mtapata shida wananchi lakini ni lazima tutoe fursa ya kufanya inforcement ya Sheria zetu.  Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, wafanyabiashara ya mafuta wana maneno matamu sana, watakuambia kuhusu profit margins zao lakini muwaulize wakati tumeamua bei ya mafuta ya taa ipande the next day walipandisha bei.  Hawakutueleza masuala ya profit margins  zao.  Hawawezi kutueleza sasa masuala ya profit margins. 
Sheria imeshatoka EWURA wana kazi ya ku-enforce na sijasikia kama wafanya biashara wamefuta  wamekata rufaa, sijasikia kama Tume ya Ushindani imekaa kuangalia rufaa ambayo wafanya biashara ambao wamefutwa. Wanataka kutuonyesha ubabe wao.  Wanataka kutumia jeuri yao ya fedha.  Watanzania siku zote ni maskini jeuri.  Leo mafuta yatoke.  EWURA wa-oder mafuta yatoke.   Ikifika saa 12 jioni wafanya biashara wamegoma wanyang’anywe leseni mara moja.   Jeshi la Wanajeshi liingie wafungue vituo, wafungue ma-godown mafuta yatoke watu wetu wapate mafuta.  

Wachumi, Tume ya Mipango, Wizara ya Fedha, wakae waangalie hilo suala la profit margin la wafanya biashara wakati raia wanapata mafuta.  Hatuwezi kukaa hapa tunajadiliana mambo ya nchi kuna watu wachache wamekaa wanaamua kutokana na maslahi yao ya kibiashara.  Hatuwezi kukubali hata siku moja. 
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba nichangie na ninaomba Bunge lako tukufu likubaliane nami EWURA wafanye kazi hiyo na tuwape nguvu EWURA, vijana wetu wanapokuwa kazini tusiwakatishe tamaa. Tusiwaone EWURA ni wakosaji wakati wanatekeleza maagizo ya Bunge.  Ni sawa sawa na askari wako yuko jeshini kuna matatizo unaanza kumlaumu.  Tuwalaumu baadaye, tuwape nguvu EWURA wafanye enforcement mafuta yapatikane, twende wananchi wetu wafanye kazi kama jinsi inavyotakiwa.  Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

No comments: