![]() |
Bondia Cannavaro Akizuiwa asifanye maafaa |
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imeipa Coastal Union ushindi wa pointi tatu na mabao matatu
baada ya Yanga kumchezesha mchezaji Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye mechi kati
ya timu hizo iliyochezwa Machi 31 mwaka huu Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Uamuzi huo ulifanywa na Kamati ya Ligi iliyokutana
jana (Aprili 2 mwaka huu) kupitia ripoti mbalimbali za Ligi Kuu na Ligi Daraja
la Kwanza umezingatia Kanuni ya 25(f) ya Ligi Kuu ya Vodacom juu ya Udhibiti wa
Wachezaji.
Kanuni hiyo inasema: “Ni lazima kwa klabu na
wachezaji kutunza kumbukumbu za kadi. Klabu itakayomchezesha mchezaji mwenye
kadi tatu (3) za njano au kadi nyekundu itapoteza mchezo na timu pinzani
itapewa ushindi wa pointi tatu (3) na mabao matatu (3), iwapo mchezaji atacheza
akiwa haruhusiwi kucheza kwa ajili ya kadi tatu (3) za njano au kadi nyekundu
timu yake itapoteza mchezo. Endapo klabu haina uhakika au inataka taarifa ya
idadi ya kadi zake itaomba kwa maandishi toka TFF.”
Cannavaro alioneshwa kadi nyekundu kwa kosa la
kupiga kwenye mechi kati ya Yanga na Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu ambapo
kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ya Ligi hiyo anastahili kukosa mechi tatu.
Mchezaji amekosa mechi mbili tu.
Pia klabu za Coastal Union na Yanga zimepigwa faini
ya sh. 500,000 kila moja kwa washabiki wake kutupa chupa za majini uwanjani
wakati wa mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 32(1).
Kamati ya Ligi pia imemuondoa Kamishna wa mechi hiyo
Jimmy Lengwe kwenye orodha ya waamuzi kutokana na upungufu uliopo kwenye ripoti
yake ambapo baadhi ya matukio makubwa hakuyaripoti. Moja ya matukio hayo ni
kocha wa Coastal Union, Jamhuri Kihwelo kuzozana na mshambuliaji wa Yanga,
Hamis Kiiza.
Vilevile waamuzi wa mechi namba 151 kati ya African
Lyon na Simba wameandikiwa barua ya onyo kwa kupata alama za chini. Waamuzi hao
ni Hashim Abdallah, Abdallah Selega, Hamis Chang’walu na Hassan Mwinchum. Naye
Kamishna wa mechi namba 153 kati ya Moro United na Villa Squad, Arthur Mambeta
amepewa onyo kutokana na upungufu katika ripoti yake.
No comments:
Post a Comment