Tuesday, September 06, 2011

Kesi dhidi ya Mbunge Lema yaanza kunguruma


 
KESI ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Arusha Mjini kupitia tiketi ya Chadema, Godbless Lema, jana ilianza
kunguruma katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha kwa mawakili wa utetezi kuomba
ifutiliwe mbali  kwa madai kuwa  walalamikaji hawana haki kisheria kupinga matokeo hayo.

Kesi hiyo namba 13 ya mwaka 2010,  imefunguliwa na wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaodai kuwa Lema alitoa lugha za kashfa na ubaguzi wa kidini na kijinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa chama chao, Dk Batilda Buriani. Walalamikaji hao wanadai kuwa lugha hizo ziliathiri matokeo ya uchaguzi katika Jimbo la Arusha Mjini.Wanaompinga Lema katika kesi hiyo ni, Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo ambao kwa pamoja wanawakilishwa na mawakili Alute Mughwai na Modest Akida.

Wanadai kuwa  katika siku na
sehemu mbalimbali,  Lema alidai kuwa Dk Burian, ameolewa Zanzibar na kwamba yeye na mumewe angekwenda kuishi visiwani humo baada ya uchaguzi.

Wanadai kuwa Lema pia alitoa madai kuwa mgombe huyo wa CCM hakuwa mwaminifu na kwamba hiyo inadhihirishwa na kitendo cha kazaa na mwanamume mwingine.

Mawakili wa utetezi Method Kimomogoro, anayemwakilisha Lema,ameweka pingamizi tatu na kumuomba Jaji Aloyce Mujuluzi  kulitupilia mbali kesi hiyo kwa madai kuwa walalamikaji wameshindwa kubainisha wanavyohusika na maneno yanayodaiwa kutamkwa na mteja wake dhidi ya Dk Burian.

“Wadai hawana sababu za kisheria za kulalamika kwa sababu maneno wanayodai kutolewa kwenye mikutano ya hadhara (kama yalitolewa),yalilengwa kwa Dk Burian binafsi na si wao. Hawajaeleza madhara waliyopata wao kama wapiga kura,” alisema wakili Kimomogoro.

Hoja hiyo ilimfanya Jaji Mujuluzi kumuuliza wakili huyo, “ina maana unalenga kusema pilipili usizokula  zakuwashia nini,”

Kwa upande wake wakili Kimomogoro alijibu kuwa ndiyo alikuwa na maana hiyo.Alitaja kifungu cha 111 (1) ya sheria ya uchaguzi inayoelekeza mdai au mlalamikaji katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi, kubainisha wazi makosa ya kisheria yaliyotendeka na madhara aliyopata, jambo ambalo alidai kuwa
walalamikaji wameshindwa kufanya kupitia katika hati yao ya madai.

Wakili huyo alisema kisheria wadai hawana haki kulamikia taratibu za kampeni kulingana na sheria ya maadili ya uchaguzi iliyosainiwa na vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 mwaka jana.

Alidai kuwa sheria hiyo inatoa nafasi kwa chama au mgombea pekee kuwasilisha malalamiko katika
kamati ya uchaguzi ngazi husika ndani ya saa 48 tangu tukio lilipotokea.

Kwa upande wao, mawakili wa serikali wanaomwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mdaiwa wa pili katika shauri hilo, Timon Vitalis na Juma Masanja, waliunga mkono hoja za Kimomogoro na kwamba ushindi wa
Lema, ulionyesha matakwa na maslahi ya umma hivyo wadai lazima waonyeshe yamewaathiri vipi.

“Matokeo ya uchaguzi huonyesha matakwa ya walio wengi. Ili matokeo ya uchaguzi yatenguliwe, lazima wadai waonyeshe wameathirika vipi na hayo
matokeo ambayo ni maslahi ya umma. Hati ya madai inaonyesha maneno yalitamkwa dhidi ya Dk Burian na si wao,” alisema wakili Vitalis akiomba shauri hilo litupwe.

Alisema kifungu cha 111 cha sheria ya uchaguzi kinatoa haki kwa mpiga kura kupinga matokeo, lakini lazima azingatie sababu zinazoweza kusababisha matokeo kutenguliwa zilizoanishwa katika kifungu cha 108 cha sheria na kwamba hoja ya Dk Burian kuzaa na mwanamume mwingine haiangukii  katika kifungu hicho bali inastahili kushughulikiwa kama kashfa binafsi.

Baada ya upende wa utetezi kuwasilisha hoja za pingamizi, wakili wa wadai, Mugwai aliomba mahakama iwape muda wa kupitia na kujibu hoja, ombi ambalo  lilikubaliwa na Jaji Mujuluzi.

Baadaye, jaji huyo aliahirisha kesi hiyo hadi leo atakapoendela.

No comments: