Na Ramadhan Semtawa
MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amebainika kuwa na vijidudu 150 vya
malaria ambavyo vimemfanya alazwe Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji
Uangalizi Maalumu (ICU), katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Wakati
Zitto akilazwa ICU ndogo (Min ICU), mbunge wa Viti Maalumu (CUF),
Claradiana Mwatuka, naye amelazwa katika kitengo hicho akisumbuliwa na
vidonda vya tumbo.Jana uchunguzi kuhusu Zitto ulibaini kuwa anasumbuliwa
na malaria kutokana na kuwa na wadudu hao ambao ni wengi kwa mtu kuweza
kuwahimili.Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili jana wodini hapo
kuhusu hali yake, Zitto alisema kwa kifupi tu, "naendelea vizuri,
najisikia vizuri".
Awali, taarifa kutoka hospitalini hapo zilisema
Katibu Mkuu Wizara ya Afya alipiga marufuku Zitto kusumbuliwa na
kuagiza wote ambao walikuwa wakienda wasimsemeshe kwa muda mrefu wa
dakika 20.
Kwa upande wake, Msemaji wa hospitali ya Muhimbili,
Jezza Waziri, alisema Zitto baada ya kufanyiwa vipimo tangu alipofika
hospitalini hapo amebainika kuwa na vijidudu hivyo 150.Hata hivyo,
alisema uchunguzi zaidi kuhusu afya ya Zitto unaendelea na kuongeza
kwamba majibu ya vipimo zaidi yataonyesha kama kuna matatizo mengine au
la.
Alifafanua kuwa hadi sasa madaktari wamebaini tatizo kubwa
linalomsumbua mbunge huyo ni malaria na kuongeza kwamba jitihada na
taratibu zaidi za matibabu zimekuwa zikiendelea.
Kumpeleka India
Spika
wa Bunge, Anne Makinda jana jioni aliwaambia waandishi wa habari hapo
Muhimbili kwamba Zitto alikuwa akiendelea vizuri, lakini tatizo la
kichwa kuuma lilikuwa bado linamsumbua.Makinda ambaye alienda kumjulia
hali Zitto, alisema kutokana na tatizo hilo kuendelea, Ofisi ya Bunge
inafanya taratibu ili apelekwe India kwa uchunguzi zaidi.
Makinda
aliwataka Watanzania waendelee kumuombea ili aweze kupona.Taarifa za
watu wa karibu na Zitto zinasema kwamba huenda akasafirishwa kwenda
India kesho kwa ajili ya uchunguzi huo alioutangaza Spika Makinda.
Mbunge Mwatuka
Kuhusu
hali ya mbunge Mwatuka, Waziri alisema alifikishwa hospitalini hapo
juzi saa 4:00 usiku akisumbuliwa na matatizo ya vidonda vya tumbo na
kwamba hadi jana alikuwa akiendelea na matibabu.Alifafanua kwamba,
mbunge huyo baada ya kufikishwa hospitalini hapo alianza kupatiwa
matibabu ambayo alisema yanaendelea vizuri.
Kaka wa Zitto
Kwa
upande wa kaka wa Zitto, Salumu Mohamed alifafanua kwamba kipindi chote
ambacho ndugu yake alikuwa Aga Khan haikuweza kubainika mara moja iwapo
ana wadudu 150 wa malaria.Hata hivyo, alisema baada ya kufika ICU
Muhimbili moja kwa moja alifanyiwa vipimo vya awali ambavyo
vilivyoonyesha kwamba alikuwa na kiasi hicho cha vijidudu.
"Baada
ya kufika hapa juzi alipelekwa moja kwa moja ICU na kuchukuliwa vipimo.
Matokeo ya awali, yanaonyesha ana malaria 150, hawa ni wadudu wengi
sana," alifafanua Kabwe.Alisema bado uchunguzi zaidi kuhusu afya ya
mdogo wake unaendelea kwani bado anasumbuliwa na tatizo la kuumwa na
kichwa.
Salum alisema kama kutakuwa na umuhimu wa tatizo hilo kwenda kutibiwa nje itafahamika na itafanyika hivyo.
Wodini alikolazwa
Isipokuwa
watu maalumu tu, watu wengine hawakuwa wakiruhusiwa kuingia alikolazwa
mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwani hata
waandishi wa habari waliofika hosipitalini hapo walizuiwa kuingia wodini
hapo.
Kulikuwa na utaratibu maalamu kwani hata kwa wale
walioruhusiwa walikuwa wakihojiwa kwanza, kwamba unatoka wapi na
unamfahamu vipi mbunge huyo ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).
Wabunge mbalimbali wakiwamo
Dk Hamis Kigangwallah wa Nzega na Dk Maua Daftari wakiwa na wafanyakazi
wengine wa Ofisi ya Bunge, walikuwa miongoni mwa waliofika wodini hapo
jana.
No comments:
Post a Comment